TATIZO Inaonekana kama kwamba Nje kuna giza lenye mwanga Na ndani kuna mwanga wenye giza Nami nimekaa pasi mwanga wala giza Ni kama noana kama sioni Nimeinama kichwa karibu kama mjinga Karibu kama mwerevu. Kusoma siwezi Kuandika siwezi. Nimeshindwa kujua Ninachojua. Lakini kitu hiki ni kama Nakiogopa kama sikiogopi
Wahenga Wenye Hekima Wahenga husema ulio juu huendeshwa na ulio ndani. Ukituma watoto wadogo shambani mavuno yatakuwa ya kitoto. Ukishindwa kurudi na kware rudi na bundi. Ila kumbuka sisimizi hukusanyika sehemu yenye mfupa. Ila ndege mwoga ndiye huwa na makinda wengi . Ndama huzaliwa na masikio na pembe huota baadaye Mwewe hushinda angani lakini jion ikifika hulazimika kutua porini. Wengine husema mvua inapotokea kibandani haina pa kukimbilia ila ipo siku msitu Utakuwa na masikio. Mlima usiosikia huungua watu wakiutazama. leo ngoja nifike kwa wahenga ili tuweze kujadili ila kila ngoma ina mwisho wake